Alhamisi, 15 Januari 2015

Saratani ya tezi due:Nani yuko hatarini kuugua, afanye nini?



Mengi yamesemwa kuhusu saratani za aina mbalimbali katika jamii na athari zake kwa maisha ya binadamu.
Pia, zimekuwa zikitajwa aina mbalimbali za saratani ambazo zinawasumbua wengi katika jamii yetu.
Miongoni mwake ni  ile  ya tezi dume ambayo wanataalam wanaeleza kuwa inashika nafasi ya tatu kwa kusababisha vifo vingi nchini.

Pia, wanaume wanaokunywa pombe kupita kiasi na wale wanaofanya kazi viwandani wakitajwa kuwa katika hatari zaidi ya saratani hii.

Imeelezwa kuwa wanaume wanaofanya kazi katika viwanda vya rangi au wanaofanya kazi za kupaka rangi wamo hatarini zaidi.

Hata hivyo, saratani ya aina hii kwa wanaume inashika nafasi ya kwanza kwa kusababisha vifo vingi hapa nchini.

Aidha,saratani ya tezi dume ni chanzo kikuu cha vifo vinavyosababishwa na saratani kwa wanaume wa umri miaka 70 na kuendelea.

Hata hivyo, ni nadra kwa saratani hii kuwapata wanaume chini ya umri wa miaka 40.
Mwathirika wa saratani hiyo, na mwanzilishi wa kampeni ya kuangamiza saratani ya tezi dume ya ‘50 Plus Campaign’ Dk Emmanuel Kandusi anasema saratani hii ikitambuliwa mapema huweza kutibika.
Anasema “Kutokana na ugonjwa huo kuwa hatari hapa Tanzania, ifikapo mwaka 2020 unatarajiwa kuua watu milioni 20,”

Kwa kawaida saratani ya aina hii hukua taratibu ingawa baadhi hukua kwa kasi. Seli za saratani wakati mwingine husambaa katika maeneo mengine ya mwili hasa katika mifupa na tezi za limfu.
Saratani hii inasababisha maumivu makali hasa wakati wa kukojoa.

Wengi hushindwa kushiriki tendo la ndoa, au kukosa kabisa nguvu za kiume.

Walioko hatarini kupata saratani ya tezi dume
Watu walio katika hatari kubwa ya kupata saratani ya tezi dume ni pamoja na:
•    Wanaume wenye asili ya Afrika (Weusi) ikilinganishwa na Wazungu
•    Wanaume kuanzia miaka 60 na kuendelea.
•    Wanaume wenye historia ya tatizo hili kwenye familia zao, yaani, wale ambao mmoja wa ndugu zake (kaka au mdogo wa kiume) au baba amewahi kuugua ugonjwa huu.
•    Wakulima wanaotumia aina fulani ya mbolea za kemikali.
•    Wanaofanya kazi katika viwanda vya kutengeneza matairi.
•    Wachimbaji wa madini, hususan aina ya cadmium.
•    Walaji wa chakula chenye kiasi kikubwa cha mafuta hasa ya wanyama.

Mtandao wa Wikipedia unaeleza kuwa tafiti ziliwahi kufanyika na kubaini kuwa watu waliowahi kufanya mapenzi katika umri mdogo wapo katika hatari ya kupata saratani hii.

Aidha, utafiti huo unaonyesha kuwa magonjwa ya zinaa huweza kusababisha baadhi ya kesi za saratani hii.
Dalili za saratani ya tezi dume

Katika hatua zake za awali, dalili za saratani ya tezi dume hazitofautiani  na zile za kuvimba kwa tezi dume (BPH). Dalili hizo ni pamoja na
•    Kupata shida unapoanza kukojoa
•    Kutiririka kwa mkojo baada ya kumaliza kukojoa.
•    Kukojoa mkojo wenye mtiririko dhaifu
•    Kukojoa mara kwa mara hasa nyakati za usiku
•    Kujikakamua wakati wa kukojoa na kushindwa kumaliza mkojo wote
•    Kutoa mkojo uliochanganyika na damu
•    Kutoa shahawa zilizochanganyika na damu
Vipimo vya saratani ya tezi dume

Utambuzi wa saratani ya tezi dume hujumuisha kufahamu dalili alizo nazo mgonjwa pamoja na vipimo
Digital Rectal Exam: Daktari ataingiza kidole cha shahada katika puru (rectum) ili kuhisi tezi dume kupitia ukuta wa puru. Aidha, atahisi pia sehemu zote zinazozunguka tezi dume kutambua iwapo tezi ni ngumu au kama ina uvimbe wowote.

Aidha, kipimo hiki  ni rahisi na kisicho na gharama kuweza kugundua tatizo mapema lakini kimekuwa kikipata upinzani mkubwa toka kwa wagonjwa kutokana na imani potofu na kutokuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu kipimo hiki wakidhani ni cha udhalilishaji wa uanaume wao.
•    Kipimo cha damu kuchunguza Prostate Specific Antigen (PSA): PSA ni aina ya protein inayozalishwa na seli za tezi dume. Uzalishaji wake huongezeka wakati wa BPH, tezi dume inapopata uambukizi (prostitis) , na saratani ya tezi dume.

DRE pamoja na PSA huonesha uwepo wa tatizo kwenye tezi dume, lakini vipimo hivi havina uwezo wa kutofautisha iwapo tatizo hilo linamaanisha saratani au BPH. Hivyo, basi, ili kuweza kutofautisha kati ya magonjwa hayo mawili, kipimo kiitwacho Prostate biopsy hufanywa.
•    Prostate biopsy: Kipimo hiki hufanywa kwa kuchukua kipande cha nyama (tishu) kutoka tezi dume kwa ajili ya uchunguzi maabara.
Kipimo kingine huitwa ‘trans-rectal ultrasound’ ambacho husaidia kuonyesha ukubwa na sura ya tezi dume lilivyo.
Ili kutambua kama saratani imesambaa sehemu nyingine za mwili vipimo vya CT scan, MRI pamoja na PET navyo vyaweza kufanyika pia

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni